Monday, September 25, 2017

NASSARY ADAI ATAJIUUZULU UBUNGE KAMA???????????????

Mbunge wa Chadema wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari ameweka rehani ubunge wake  baada ya Rais John Magufuli kumpokea aliyekuwa diwani wa chama hicho aliyejiuzulu akisema ni kwa sababu ya kuunga mkono juhudi za Rais.

Nassari amedai ana ushahidi wa kielektroniki unaoonyesha madiwani hao walivyopewa rushwa ili wajiuzulu nafasi zao.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Kimandolu, Mchungaji Rayson Ngowi ambaye amepokewa na Rais Magufuli juzi  baada ya kujiuzulu Chadema akizungumzia tuhuma hizo alisema madai hayo hayana ukweli wowote na kama Nassari ana ushahidi ni vyema angeutoa hadharani.

Ngowi aliwashauri Chadema mkoani Arusha watatue matatizo yaliyopo ndani ya chama hicho na wasitafute visingizio kwa kuwa yeye ameamua kujiuzulu kwa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na hajapewa rushwa yoyote.

Diwani mwingine aliyejiengua katika chama hicho wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe alisema hakuna chochote alichopewa kama rushwa kwa lengo la kujiuzulu, akimshauri Nassari autoe hadharani ushahidi anaousema na si kushusha tuhuma zisizo na mashiko.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Nassari alisema ushahidi huo ameuhifadhi ndani ya ‘flash disc’ na yuko tayari kumkabidhi Rais Magufuli na vyombo vya uchunguzi.

Mbunge huyo alisema endapo ikithibitika kuwa ushahidi wake ni wa uongo yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya ubunge.

“Ninao ushahidi na kama Mheshimiwa Rais yuko tayari niko tayari kumpatia ninayo flash, ushahidi ninao kwa muda mrefu na tulijua watapokelewa juzi madiwani wawili lakini mmoja amekataa akaenda mmoja,” alisema Nassari. 
 
Alidai kwamba  kwa kipindi kirefu alipokuwa masomoni nchini Uingereza alikuwa akijiuliza ni kwa nini madiwani katika Mkoa wa Arusha wamekuwa wakijiuzulu na ndipo alipoamua kufanya uchunguzi wa kina.

Nassari akiwa ameambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika mkutano huo, alisema alianza kufanya uchunguzi Mei kwa kutumia vifaa vya kielektroniki alivyovinunua nchini Uingereza na kubaini kwamba baadhi ya madiwani wanaojiuzulu walipewa rushwa ya fedha, ahadi ya vyeo na ya makazi.

Alisema uchunguzi juu ya tuhuma za madiwani hao kujiuzulu aliufanyia ndani ya ofisi ya umma akisisitiza hakuna diwani wa Chadema mkoani Arusha ambaye amejiuzulu kwa kumuunga mkono Rais Magufuli bali wamepewa rushwa.

“Mheshimiwa Rais anapambana na rushwa lakini kuondoka kwa madiwani ni mfumo wa rushwa anaopambana nao niko tayari kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge endapo ikithibitika ushahidi wangu ni wa uongo,” alisema Nassari.

Madiwani wapatao 10 wa Chadema wamejiuzulu kwa nyakati tofauti. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ameshawahi kunukuliwa akikanusha tuhuma za kupewa rushwa madiwani wanaojiengua kutoka Chadema na kujiunga na CCM.

Polepole Julai alikaririwa akisema iwapo Chadema ina viongozi wanaoweza kuhongwa na wakahongeka basi ni chama cha  ovyo kwa kuwa chama kilicho imara na watu wake wapo safi hawawezi kuhongeka.

Alitoa kauli hiyo mjini Bagamoyo alipohudhuria mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso) Mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment