Halmashauri zote nchini zimetakiwa kutenga maeneo ya michezo wakati wa
kupanga mipango miji kwa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipokuwa akifunga fainali ya mashindano ya
Jimbo Cup inayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Mhe. Mbunge wa
Mbulu Vijijini, Flatei Massay iliyochezwa katika eneo la kata ya Dongobesh
Wilaya ya Mbulu Mkoani wa Manyara.
“Natoa wito kwa Halmashauri zote ikiwemo halmashauri yenu ya wilaya ya
Mbulu wakati wa kupanga matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya mipango miji
mkumbuke kutenga maeneo ya michezo, Baraza la Michezo la Taifa litatoa mafunzo
ya michezo na utaalam” alisema Naibu Waziri Wambura.
Akikabidhi zawadi za washindi katika mashindano hayo ambao ni timu ya
Qatajiring kutoka kijiji cha tumati ambao ni mshindi wa kwanza na timu ya
Zahanati kutoka kijiji cha Diomati mshindi wa pili, Naibu Waziri Wambura
amewahimiza wachezaji na wananchi kuthamini michezo kwa kuwa ni ajira, inaleta
umoja na mshikamano miongoni mwa jamii.
Dakika 90 za fainali hizo ziliisha kwa timu zote kufungana bao 2-2 na
hatimaye timu ya Qatajiring iliibuka kidedea kwa ifunga timu ya Zahanati kwa
penati 4-1.Akionesha umuhimu na umahiri wa wilaya ya Mbulu katika michezo,
Naibu Waziri Wambura amesema wilaya hiyo imekuwa kitovu cha wanamichezo bora
hasa mchezo wa riadha ambao wameiletea sifa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Wanamichezo hao ni pamoja na John Stephen Akhwari nguli mchezo wa
riadha aliyeweka historia ya kimataifa aliyewahi kusema “Nchi yangu haikunituma
kuanza mashindano, ilinituma kumaliza mashindano”Filbert Bai na wanaridha
wengine.
Aidha, Naibu Waziri Wambura amewashauri waandaaji wa mashindano hayo
washirikishe pia mchezo wa netiboli ili kuwaendeleza watoto wa kike katika
mchezo huo.Kwa upande wake mdhamini wa mashindano hayo Mbunge wa Mbulu Vijijini
Flatei Massay amesema kuwa alivutiwa kuanzisha mashindano hayo ili vijana
wajihusishe na michezo na kuboresha na kuendeleza afya zao na kuachana na
masuala yanayoweza kupoteza maisha yao na nguvu kazi ya taifa
Mashindano hayo yalishirikisha timu 24 kutoka Mbulu Vijijini tangu
kuanzishwa kwa mwezi Julai mwaka huu na kufikia kilele Septemba 25 ambapo
fainali ilichezwa katika viwanja vya Dongobesh na kushuhudiwa na viongozi
mbalimbali na mashabiki lukuki kutoka maeneo yote ya halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment