Monday, September 25, 2017

Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Septemba, 2017 amemaliza ziara yake ya siku 6 katika Mkoa wa Arusha.

Akiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Sangsi nje kidogo ya Jiji la Arusha na wananchi wa Pacha ya Kia Mkoani Kilimanjaro na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwahudumia bila kuwabagua kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini na ukabila.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutimiza azma hiyo Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Usa River  – Arusha inayojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 139, mradi wa maji wa Arusha utakaogharimu Shilingi Bilioni 42, mradi wa kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 200 na mingine mingi inayotekelezwa katika maeneo hayo.

“Nina uhakika nyinyi wakazi wa Arusha mnaona Arusha inavyobadilika, kabla ya kujengwa barabara hii kulikuwa kunatokea ajali nyingi, na kuna watu walikufa pale kwenye daraja, inawezekana wengine wameanza kusahau, wanaozaliwa sasa hivi wanaweza kuona haya sio chochote lakini hii ni ishara ya kupanda kwa uchumi wetu, uchumi unapopanda na miundominu inakuwa mizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero mbalimbali za wananchi wakiwemo wafanyakazi ambao wamelalamikia kuhamishwa vituo vya kazi bila kulipwa stahiki zao na amerejea agizo lake la kupiga marufuku mfanyakazi yeyote kuhamishwa kituo cha kazi pasipo kulipwa stahiki zake.

Kuhusu kero za wananchi wa pacha ya Kia waliolalamikia tatizo la uhaba wa maji, kunyang’anywa maeneo ya biashara na waliokuwa walinzi wa uwanja wa ndege kudai haki zao Mhe. Rais Magufuli ameziagiza mamlaka husika kushughulikia matatizo hayo.

Mhe. Rais Magufuli amerejea Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
25 Septemba, 2017

No comments:

Post a Comment