Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe
12 Septemba, 2017 ametembelea hospitali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) Lugalo, Jijini Dar es Salaam na kumjulia hali Meja Jen.
Mstaafu Vincent Mritaba aliyelazwa hospitalini hapo baada ya
kushambuliwa na watu wenye silaha wakati akiingia nyumbani kwake Ununio,
Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Meja
Jen. Mstaafu Mritaba alishambuliwa kwa risasi jana tarehe 11 Septemba,
2017 majira ya mchana na kisha kukimbizwa katika hospitali ya Jeshi
Lugalo kwa matibabu.
Mkuu
wa kituo cha tiba cha hospitali hiyo na daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo Brigedia Jenerali Paul Massawe amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa
Meja Jen. Mstaafu Vincent Mritaba anaendelea vizuri baada ya madaktari
kufanikiwa kutoa risasi alizopigwa mkononi, kiunoni na tumboni.
Meja Jen. Mstaafu Mritaba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumjulia hali na kumuombea dua ili apone haraka.
Mhe.
Rais Magufuli aliyeongozana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jen. Venance
Mabeyo pia ametembea wodi ya majeruhi na kuwajulia hali wagonjwa
wanaotibiwa katika wodi hiyo na baadaye akawasalimu wananchi waliofika
hospitali hapo kwa ajili ya kupata matibabu.
Mhe.
Dkt. Magufuli amewapongeza Madaktari wa hospitali ya jeshi Lugalo kwa
huduma za matibabu wanazotoa kwa askari na wananchi wengine na
amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Septemba, 2017
No comments:
Post a Comment