Wiki moja
baada ya kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia uvunjifu wa amani nchini.
Kikosi
hicho kinachoshirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama pia kinashughulika
na kukusanya silaha za kivita ambazo zimekuwa zikitumika.
Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema hayo bungeni leo
Alhamisi akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Salim
Hussein.
Mbunge
huyo amesema hana wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) katika kusimamia majukumu yake ndiyo maana nje ya mipaka ya
nchi ni salama lakini ana wasi wasi kuhusiana na hali ya usalama nchini.
“Lakini ndani
ya nchi yetu hali si salama na mifano miwili ya juzi ya mbunge (Lissu) na Meja
Jenerali mstaafu Vincent Mritaba inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna
matatizo, je ni kwa nini Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kuondosha
matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu?” Alihoji
mbunge huyo.
Amesema
anavyoona yeye silaha za kivita zinamilikiwa na JWTZ na matumizi yake
yanatakiwa yawe ya chombo hicho.
Mbunge
huyo alihoji ni kwa nini wasitumike askari maalumu kuhakikisha silaha za kivita
zinazotumika vibaya kuua raia zinakamatwa.
Waziri
Mwinyi akijibu swali hilo amesema ni dhahiri kwamba kazi ya JWTZ ni ulinzi wa
mipaka lakini pale linapohitajika au kuombwa kusaidia mamlaka zingine za kiraia
au vyombo vingine vya ulinzi na usalama huwa tayari kufanya hivyo.
“Tunavyozungumza
ni kwamba, mamlaka hizo ambazo ni vyombo vingine vya ulinzi na usalama
vikihitaji msaada wa jeshi mara zote tunakuwa tayari kutoa msaada huo, kwa hali
ilivyo sasa imeundwa task force (kikosi kazi) inayojumuisha vyombo vyote vya
ulinzi na usalama ili kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjivu wa amani ndani ya
nchi,” amesema.
Amesema
hana shaka na kazi hiyo imeanza, hivyo kuwahakikishia wananchi kuwa jukumu hilo
litafanywa vyema ili hali ya usalama iwepo ndani ya nchi.
Dk Mwinyi
amesema ni kweli silaha za kivita zinadhibitiwa na JWTZ na kwa kutumia kikosi
kazi hicho, watakusanya silaha hizo kutoka kwa raia au watu wengine wote ambao
wanamiliki silaha hizo ambazo kwa kawaida, utaratibu na kisheria hawapaswi kuwa
nazo.
Amesema
zitakapopatikana silaha hizo zitarudishwa katika mamlaka zinazohusika.
Katika
swali la msingi, Mbunge wa Mkoani (CUF), Twahir Awesu Mohamed alihoji Serikali
imejipangaje kuimarisha amani nchini.
Waziri
Mwinyi amesema JWTZ imejipanga kikamilifu kuhakikisha mipaka ya nchi inalindwa
muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.
“Jeshi
letu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeimarisha ulinzi katika
maeneo ya mipaka yenye wakimbizi ,” amesema.
Amesema
hatua hiyo imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyowezwa
kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi.
No comments:
Post a Comment