Siku moja baada ya agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa agizo kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro kufuatilia utendaji wa kampuni ya Zhong Fenq, umeviagiza vyombo vya ulinzi kuwakamata raia watatu wa China wanaodaiwa kuendesha shughuli za uwekezaji kinyume cha sheria.
Juzi, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen
Kebwe na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kwenda katika kijiji cha Maseyu kufuatilia utendaji wa kampuni hiyo kama inafuata sheria, kanuni na utaratibu.
Dk Kebwe jana alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata raia hao na kuamuru warudishwe kwao mara moja baada ya kugundulika kujihusisha na uchimbaji wa madini ya kutengeneza marumaru bila kufuata utaratibu, kanuni na sheria za nchi.
Waziri mkuu alitoa agizo hilo kutokana na malalamiko ya mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba kuwa wawekezaji hao kutoka China wanaendesha shughuli za uchimbaji bila ya kuwa na kibali.
Mgumba alisema tangu mwaka 2011 wawekezaji hao wameendesha shughuli zao bila kulipa kodi za Serikali na tozo za halmashauri, hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako jimboni kwake,
alisema licha ya uongozi wa mkoa kwenda eneo hilo na kuizuia kampuni kuendelea na uchimbaji hadi itakapopata vibali ilikaidi na kuendelea na shughuli zake.
Majaliwa alisema iwapo wahusika watabainika kuwa hawajafuata sheria, kanuni na utaratibu hatua zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika eneo hilo chini ya ulinzi na kuwasiliana na ubalozi wa China nchini.
Akitoa agizo jana, Dk Kebwe alimtaka kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro na kamanda wa Uhamiaji wa mkoa kuhakikisha wanawakamata na kuwasafirisha raia hao wa China hadi jijini Dar es Salaam na utaratibu wa kuwaondoa nchini ufanyike mara moja.
“Nawaagiza kuhakikisha mnaorodhesha vifaa na vitu vyote vilivyopo katika mgodi huo,” alisema Dk Kebwe.Raia hao wa China kwa sasa wanashikiliwa na polisi wakisubiri kukamilishwa kwa utaratibu wa kuwarudisha kwao, huku mali za mgodi huo zikiwa chini ya uangalizi wa jeshi hilo.
Katika hatua nyingine, Dk Kebwe aliagiza polisi kuwakamata mhasibu wa halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ofisa biashara, mtendaji wa kata ya Maseyu na mtendaji wa kijiji hicho kwa kushindwa kutoa taarifa za raia hao wa kigeni kuendelea na uchimbaji huo.
Pia, Dk Kebwe alisema waliendelea kuwatoza kodi ya huduma hadi Juni mwaka huu licha ya kujua kuwa hawana kibali.
Akizungumzia kuchelewa kuondoka kwa Wachina hao, ofisa madini mkazi Mkoa wa Morogoro, Bertha Luzabiko alisema mamlaka ya Wizara ya Nishati na Madini ndiyo ilikuwa ikishughulikia suala lao.
Mkuu wa uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Safina Muhindi alisema mpaka sasa hajaona pasipoti wala vibali vya kufanya kazi nchini vya rais hao, hivyo ufuatiliaji unaendelea.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema walichofanya ni kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa la kuwakamata
Mwaka 2016 mgodi huo ulizuiwa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini na uzalishaji wa marumaru baada ya kubainika kuwa wawekezaji hao hawana vibali, huku bidhaa zilizokuwa zikizalishwa na kampuni hiyo zimekuwa zikiandikwa kuwa zinatengenezwa China.
Imeelezwa uongozi wa mgodi ulisitisha shughuli kwa muda na baadaye ulirejea kuendelea na uzalishaji.
No comments:
Post a Comment