WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa kilimo na maafisa ushirika wa
mkoa wa Tabora wasimamie kwa umakini ukuzaji wa zao la tumbaku kuanzia
msimu ujao.
“Mkakati wetu wa kuinua zao hili unaanza msimu ujao, ninaondoka Tabora lakini nataka kila mmoja wenu atumie nafasi yake kuelezea suala hili kwa kina kwa wakulima wa zao la tumbaku ili tubadilishe mfumo na tuweze kuwakomboa,” alisema.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo Jumapili, Agosti 13, 2017wakati akizungumza na
watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa
huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum. Kikao hicho
kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe na baadhi ya watendaji
kutoka wizara hiyo.
Aliwataka
watendaji hao watumie vyombo vya habari vya ndani ya mkoa na vya
kitaifa kuelezea mkakati mpya ambao serikali inao wa kuinua zao la
tumbaku. “Tumieni vyombo vya habari kila mmoja apange ratiba kuelezea
atafanya nini, toeni elimu kwa sababu vyombo hivi vinasikika hadi kwenye
mikoa ya jirani,” alisisitiza.
“Afisa
kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je wakulima wako
kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana mahitaji ya
pembejeo kiasi gani?” alisema.
“Afisa
ushirika wa wilaya nawe hakikisha unasajili idadi ya vyama vya msingi
(AMCOS) vilivyoko kwenye eneo lako, lazima ujue AMCOS ziko ngapi na zina
wanachama wangapi. Afisa kilimo na afisa ushirika muanze kazi hiyo mara
moja,” alisisitiza.
“Ulizeni
mahitaji yao ni yapi, kwa kila mwanachama na kila AMCOS, kisha
muziwasilishe kwa Mkuu wa Mkoa ili naye azifikishw kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo. Pale wizarani, tunataka Mkurugenzi wa Pembejeo ajue
mahitaji ya kila mkoa ili pembejeo ziweze kuwasilishwa kwa wakulima
miezi miwili kabla msimu wa kilimo haujaanza, kama ambavyo tumeagiza,”
alisema.
Akifafanua
kuhusu uagizaji wa mbolea, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanzisha
mfumo wa pamoja wa mbolea (bulk procurement) na akawataka wataalamu wa
wizara ya kilimo wamalize mgogoro wa siku nyingi uliokuwepo baina yao na
kiwanda cha mbolea cha Minjingu.
“Kumekuwa
na maneno maneno kuhusu mbole ya NPK, lakini wakati sisi tunaidharau,
wenzetu wa nchi jirani wanaongoza kwa kuagiza mbolea nyingi kutoka
Minjingu. Acheni kuagiza mbolea hiyo kutoka nje ya nchi, tukachukue pale
Minjingu,” alisisitiza.
Alisema
mwenye kiwanda ameahidi kwamba akipewa oda ya mbolea, yeye
atazisafirisha hadi kiwandani. “Hakuna haja ya kuwaumiza wakulima na
mbolea za bei mbaya wakati tunayo hapa nyumbani na tena ya bei nafuu.
Wenye makampuni ya kununua tumbaku wanauza mfuko mmoja kwa dola 70 sawa
na sh.150,000 hii ya Minjingu yenye ubora uleule inauzwa sh. 60,000 kwa
mfuko mmoja, tena zikiwa zimefikishwa wilayani.”
“Ninawasihi
viongozi wa ushirika na wa wilaya tusaidiane kumuondoa mkulima kwenye
utegemezi wa mikopo ya benki na badala yake tuwaelimishe wajiwekee akiba
ya kumudu pembejeo za msimu unaofuata,” alisisitiza.
Alisema
kama kutakuwa na ulazima wa kuingia kwenye mikopo, viongozi hao hawana
budi kuhakikisha kuwa wanaisimamia kwa kikamilifu. “Kama mtaingia kwenye
mikopo, lazima mjipange kuisimamia mikopo hiyo ili isije ikawarudisha
nyuma wakulima wetu kwenye mfumo ambao ulikuwa unawaumiza,” aliongeza.
Akifafanua
kuhusu ununuzi wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema AMCOS ndizo zenye
tumbaku na kwa maana hiyo ndiyo zitahusika na uuzaji. Katika kila
wilaya, wekeni mfumo wa usimamizi kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Malori yakikamatwa na marobota yaliyouzwa nje ya mfumo, ni lazima hatua
kali zichukuliwe,” alisisitiza.
“Ninasema
hakuna mazungumzo tena nje ya AMCOS, ni kwa kampuni ya ununuzi au kwa
mtu binafsi. Na kuanzia sasa, Associations za tumbaku zimefutwa. Mkuu wa
Mkoa na wakuu wa wilaya hakikisheni hakuna associations kwenye zao la
tumbaku, tunataka kila mmoja akanunue kwenye AMCOS na kila mkulima
asajiliwe kwenye AMCOS,” alisisitiza.
Alisema
Serikali ilivunja Chama Kikuu cha Ushirika Kanda ya Magharibi (WETCU)
kutokana na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na viongozi wa chama hicho na
kwamba hivi sasa kutakuwa na WETCU mbili ambapo ya kwanza (WETCU I)
itahusika na wilaya za Kaliua na Urambo na ile ya pili (WETCU II)
itahudumia wilaya za Sikonge, Uyui, Nzega na sehemu ndogo ya Tabora
Manispaa.
Alisema
hatua hiyo imechukuliwa ili kuwe na vyama vikuu viwili vyenye AMCOS
chache lakini zenye uwezo wa kuwafikia wakulima, kusikiliza mahitaji yao
na kutatua matatizo yao. WETCU ya zamani ilikuwa na AMCOS 214 na
haikuweza kuwafikia wakulima wote.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 14, 2017.
No comments:
Post a Comment