Saturday, August 12, 2017

Marekani Kupitia Shirika Lake La Misaada La USAID Yaipatia Tanzania Dola Milioni 225 Kwa Ajili Ya Miradi Mbalimbali Ya Maendeleo


Siku moja baada ya Marekani kutangaza kutoa fedha za nyongeza katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini, nchi hiyo imetiliana saini na Wizara ya Fedha na Mipango makubaliano ya kutoa Dola Milioni 225. 
 
Fedha hizo zitaelekezwa katika sekta mbalimbali zikiwemo Elimu, Afya, Kilimo na Utawala bora.
 
Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo imefanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) hapa nchini Bw. Andy Karas.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano hayo Bw. Doto James ameishukuru Marekani kwa kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na Tanzania na amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha juhudi za Serikali kuwaletea maendeleo wananchi.

Nae Bw. Andy Karas amesema Serikali na watu wa Marekani wanafurahishwa na kuendelea kwa ushirikiano mwema kati yao na Serikali ya Tanzania katika maendeleo na ameahidi kuwa ushirikiano huo utadumishwa.
 
Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo imehudhuriwa na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson ambaye amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo.

No comments:

Post a Comment