Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili
nchini Afrika ya Kusini tayari kwa kuhudhuria Mkutano wa 37 wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC
unaoaanza tarehe 19 na 20 ambapo kesho tarehe 18 atahudhuria Mkutano wa
Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika Mbili ya SADC (SADC
Double Troika Summit).
Mheshimiwa Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan amepokelewa na Waziri wa Mawasiliano wa Afrika Kusini Mhe.
Ayanda Dlodlo, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli
Akizungumza mara baada ya
kuwasili kwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augastine Mahiga amesema Mkutano huo
utapokea na kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wa SADC na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama;
Hali ya Michango mbalimbali ya Nchi Wanachama na Kupokea taarifa ya
Mwenyekiti anayeondoka wa SADC Organ.
Pia Mkutano utapokea
taarifa ya Katibu Mtendaji wa SADC; Kupitia hali ya kiuchumi katika
Kanda ya SADC; Kuwasilisha Kaulimbiu ya Mkutano wa SADC; Taarifa kuhusu
Mfuko wa Maendeleo wa SADC; Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Viwanda; Kuwezesha Chuo cha Elimu ya Sayansi na Teknolojia; Maombi ya
Serikali ya Comoro na Serikali ya Burundi kujiunga na SADC; Utekelezaji
wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika na Mkutano wa Mshikamano
kati ya SADC na Saharawi ya Magharibi. Dkt. Mahiga amesema
katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika Mbili
ya SADC (SADC Double Troika Summit) Tanzania itakabidhi nafasi ya
Uenyekiti kwa Mwenyekiti mpya.Double Troika inahusisha nchi
wanachama sita ambao kwa sasa ni Swaziland, Tanzania, Afrika Kusini,
Angola, Botswana na Msumbiji. Katika mkutano huo Mfalme Mswati III wa
Swaziland atakuwa ndiye Mwenyekiti.
Ajenda kuu katika Mkutano huu ni
kupokea na kujadili taarifa kuhusu hali ya kisiasa, kiulinzi na
kiusalama katika Kanda na hasa nchini DR Congo na Lesotho.
No comments:
Post a Comment