Wednesday, August 9, 2017

KOREA KASKAZINI YAJIPANGA KURUSHA MAKOMBORA KARIBU NA KISIWA CHA MAREKANI.........TRUMP AJIBU, ADAI DUNIA NZIMA ITATIKISIKA

Korea Kaskazini imedokeza kwamba inatafakari uwezekano wa kurusha makombora karibu na jimbo la Marekani la Guam katika bahari ya Pasifiki, saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitishia Pyongyang kwamba itakabiliwa kwa "moto na ghadhabu".

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini limesema taifa hilo linatafakari mpango wa kurusha makombora ya masafa ya kati na mbali karibu na Guam, eneo ambalo Marekani huwa na ndege zake za kuangusha mabomu.
Taarifa hiyo inaashiria kuongezeka kwa uhasama kati ya nchi hizo mbili. Umoja wa Mataifa hivi majuzi uliidhinisha vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo.
Rais Trump ametoa tamko lake baada ya ripoti kwenye vyombo vya habari kusema kwamba Korea Kaskazini imeweza kuunda kichwa cha silaha za
nyuklia chenye uwezo wa kutosha kwenye makombora yake.
Ufanisi huo, ingawa haujathibitishwa rasmi, ulitazamwa na wengi kama kiunzi cha mwisho kilichoizuia Korea Kaskazini kuwa taifa kamili lenye nguvu za silaha za nyuklia.
Taarifa ya gazeti la Washington Post, ikunukuu maafisa wa ujasusi wa Marekani, imedokeza kwamba Korea Kaskazini inaunda silaha za nyuklia zenye uwezo wa kuishambulia Marekani kwa kasi zaidi ya iliyotarajiwa.
Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limesema jeshi la nchi hiyo "linachunguza kwa makini mpango wa kuanzisha moto wa kuzingira Guam kwa kutumia makombora ya roketi ya masafa ya wastani na ya masafa marefu ya Hwasong-12".
Shirika hilo limesema mpango huo utawasilishwa kwa Viongozi Wakuu baada ya "kutathminiwa kwa kina na kukamilishwa" na utatekelezwa kiongozi wake Kim Jong-un akiamrisha, shirika la habari la Korea Kusini la Yonhap limeripoti.
Majibizano kati ya Marekani na Korea Kaskazini yamezidi baada ya Pyongyang kufanyia majaribio makombora mawili yenye uwezo wa kusafiri kutoka bara moja hadi nyingine, na kudai kwamba sasa ina makombora yanayoweza kufika Marekani .

Bwn Trump aliwaambia wanahabari Jumanne kwamba: "Korea Kaskazini wasithubutu kutoa vitisho zaidi kwa Marekani. Watajibiwa kwa moto na ghadhabu ambayo ulimwengu haujawahi kushuhudia."
Seneta mkongwe wa Marekani John McCain hata hivyo alikuwa na shaka kuhusu tamko la Trump.
"Viongozi wengi wakuu ambao nimewahi kuwaona, huwa hawatoi vitisho ikiwa hawako tayari kuvitekeleza na sina uhakika kwamba Rais Trump yuko tayari kuchukua hatua," alisema Bw McCain.
Korea Kaskazini ilikuwa imeghadhabishwa na vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi.
Vikwazo hivyo vina lengo la kupunguza mapato kutoka kwa mauzo ya bidhaa nje ya Korea Kaskazini kwa theluthi moja.
KCNA imesema Korea Kaskazini, ambayo imefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano, itajibu vikali na kwamba "Marekani italipia" kwa kuchangia kutunga vikwazo hivyo.


Credit:BBC

No comments:

Post a Comment