Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amekataa ombi la wabunge wa Ulyankulu na Kaliua ya
mkoani Tabora ya kuigawa Wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa
wananchi waishio kwenye kata na tarafa zilizo mbali.
Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Serikali kutamka hadharani kwamba hawatagawa maeneo mapya utawala.
Julai
mwaka jana akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa huo, Rais John
Magufuli pia alikataa ombi la kuugawa Mkoa wa Tabora akisema haoni
umuhimu wa kufanya hivyo na badala yake fedha hizo zielekezwe katika
kuboresha miundombinu ya barabara, maji na huduma za afya.
“Nataka
huduma kwanza mkoa baadaye, huwezi ukaigeuza kila wilaya ikiwa mkoa.
Kila unapotengeza mkoa Serikali inaingia gharama. Ninataka niseme ukweli
ni nafuu tutekeleze ahadi kwanza,” alisema Rais Magufuli katika ziara hiyo.
Awali,
Februari mwaka huu, Rais Magufuli aliridhia kuanzishwa kwa wilaya mpya
za Songwe, (Mkoa wa Songwe), Kibiti (Pwani), Kigamboni na Ubungo (Dar es
Salaam), Malinyi (Morogoro) na Tanganyika (Katavi).
Kabla
ya kutangaza wilaya hizo, mwaka 2015, Serikali iligawanya baadhi ya
majimbo mbalimbali kutokana na ukubwa na kupata majimbo mapya 26.
Miongoni
mwa majimbo hayo ni Kibamba, Kigamboni, Makambako, Butiama, Tarime
Mjini, Bunda Mjini, Tunduma, Newala Mjini, Mbagala, Vwawa, Mafinga
Mjini, Nanyamba, Handeni Mjini, Ushetu, Nzega Mjini, Ndanda na Madaba.
Jana,
akiwa katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Ulyankulu na Kaliua ikiwa
ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tabora, Majaliwa
aliwaambia wananchi na wabunge hao kwamba Serikali imesitisha mchakato
kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.
Akijibu
maombi ya wabunge hao Magdalena Sakaya (Kaliua) na John Kadutu
(Ulyankulu), ambao walisema kuna haja ya kuigawa Wilaya ya Kaliua ili
kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa
Majaliwa alisema, “Tumesitisha kutoa maeneo mapya ya utawala ili
tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya
majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na halmashauri mpya,
zikitengamaa tutafanya uamuzi upya.”
Kuhusu
migogoro baina ya wanavijiji na maeneo ya hifadhi, Majaliwa alisema
Serikali bado inafanya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na
ikikamilisha mchakato huo na itatoa taarifa.
Ili
kuharakisha mchaktato huo, Majaliwa aliwataka wananchi wanaoishi
pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi wasifanye
upanuzi wowote hadi uhakiki wa mipaka utakapokamilika.
“Tumeamua
kuweka beacons katika maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita
wapi. Wananchi mkiwaona watu wa hifadhi wanapita huko msigombane nao.
Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya mipaka,” alisema.
Awali
Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alimweleza Majaliwa kwamba
wananchi wanashindwa kujenga makazi ya kudumu katika maeneo waliyopo kwa
sababu wanatishiwa kwamba wapo hifadhini.
Hata
hivyo, Majaliwa alisema Serikali inafanya mapitio na ikilazimu, itabidi
ifanye marekebisho ya sheria inayohusu Misitu ya Hifadhi pamoja na
sheria inayohusu masula ya wakimbizi.
No comments:
Post a Comment