Rais
Uhuru Kenyatta huenda akaingia katika vitabu vya kumbukumbu na historia
kwa marais wa Afrika kwa kuamua kuruhusu maandamano ya amani kupinga
ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Kenyatta amewataka polisi kujizuia kutumia nguvu kubwa na badala yake wawape ulinzi wakati wa maandamano hayo ya amani na yanayoruhusiwa kisheria kwa watu ambao hawafurahii matokeo ya uchaguzi uliopita.
Rais
Kenyatta alisema hayo jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa wagombea
walioshindwa katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne iliyopita.
Kenyatta alisema hayo akiwa Jengo la Harambee alikokwenda kukutana na Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya kuapishwa kwake.
Katika
ujumbe huo uliomlenga zaidi Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais
kupitia muungano wa Nasa, Kenyatta aliwataka wagombea wote ambao
hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi wachukue hatua zilizobainishwa na
Katiba ili kupata wanachotaka.
“Marafiki
zetu ambao hawataki kukubaliana na matokeo ... tumenyosha mkono wetu wa
udugu kwao ... watumie njia zozote zilizobainishwa katika katiba
kuelezea kutoridhishwa kwao,” alisema.
“Wale
wanaotaka kushawishi wengi wagome wanaweza kufanya hivyo, lakini kwa
kuzingatia vifungu vya sheria. Mwishoni mwa siku sisi sote ni Wakenya.
Hakuna haja ya kudhuriana. Hakuna haja ya kuharibiana
mali...tunawashukuru polisi kwa kazi nzuri lakini waendelee kujizuia.”
“Polisi
wako tayari kuwalinda wakati mnafanya maandamano na wale waliochukia
waelewe kwamba hawahitaji kibali changu wala cha Jubilee kufanya
maandamano ya amani.”
Hata
hivyo, alitoa onyo kali kwamba serikali haitavumilia maandamano
yatakayosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu kutokana na vurugu.
Vilevile
alitoa onyo dhidi ya waporaji na waharibifu wa mali katika baadhi ya
maeneo ya nchi, ambako yameripotiwa maandamano baada ya uchaguzi.
“Wakenya
wengi wamesema uchaguzi umepita na wamerejea kazini. Hawataki
maandamano ya ghasia. Msivuruge maisha ya watu wengine. Kama serikali
hatutaruhusu uharibifu wa mali wala upotevu wa maisha na uporaji.”
Rais
Uhuru alitoa kauli hiyo baada ya viongozi wa muungano wa Nasa
kuhamasisha wafuasi wao kukataa matokeo yaliyompa ushindi Uhuru na
makamu wake, William Ruto.
Baada
ya kazi ya kuhesabu kura kukamilika, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
(IEBC) ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi kwa kura 8,203,290 sawa na
asilimia 54.27.
IEBC
ilisema mgombea urais kwa muungano wa Nasa, Raila Odinga alipata kura
6,762,224 sawa na asilimia 44.74 matokeo ambayo wanayapinga.
Wakiitikia
wito wa viongozi wao kati ya Jumatano na Jumamosi maeneo, ambayo ni
ngome ya upinzani ya Kisumu, Kibera, Homabay na Migori yalikumbwa na
vurugu na soko la Garissa lilichomwa moto.
Nasa
walidai kwamba, kwa mujibu wa vyanzo vyao kutoka ndani ya IEBC Raila
alishinda kwa kura milioni nane akifuatiwa na Uhuru. Walidai wizi huo
ulifanikishwa kwa kudukua kompyuta iliyokuwa inahifadhi matokeo na
kumbukumbu nyingine.
Juzi,
akizungumza na wafuasi wake waliojitokeza kwa wingi katika eneo la
Kibera, Raila aliwataka wafuasi wake wote kususia kazi jana ili
kuomboleza vifo vya waliouawa katika makabiliano na polisi.Pia, alisema
atatoa msimamo leo wa nini cha kufanya.
Katika
kile kinachoonekana kuwa ni kutii wito wa serikali, watu walionekana
kupuuza wito wa Raila wa kususia kazi kuomboleza watu waliouawa katika
makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wanapinga matokeo
ya uchaguzi wa urais.
Wengi walionekana barabarani wakirejea kwenye shughuli zao jana na kuendelea na maisha ya kawaida.
No comments:
Post a Comment