Usain Bolt amesema alikuwa
"anasema kwaheri kwa kila kitu" na alikuwa "karibu kulia"
alipokuwa anafikisha kikomo maisha yake kama mwanariadha katika mashindano ya
ubingwa wa dunia jijini London.
Bolt, 30, mshindi wa dhahabu mara nane
katika Olimpiki, amestaafu kutoka kwenye riadha baada ya kung'aa sana na
kujizolea umaarufu si haba.
"Inasikitisha kwamba inanilazimu
kuondoka sasa," alisema raia huyo wa Jamaica, ambaye alikimbia kuzunguka
uwanja kuwaaga wachezaji uwanja wa michezo wa London Jumapili usiku wa kufungwa
kwa mashindano hayo.
"Nilikuwa nasema kwaheri kwa
mashabiki na kwaheri kwa mashindano
niliyokuwa nashiriki pia."
Alipoulizwa iwapo atarejea kushindana
tena, alijibu: "Nimewaona watu wengi sana wakistaafu na kurudi tena halafu
hali yao inakuwa mbaya zaidi au wanajiaibisha.
"Sitakuwa mmoja wa watu hao."
Bolt alishinda shaba mbio zake za
mwisho za mita 100 kisha akaumia na kushindwa kumaliza mbio za kupokezana
vijiti za 4x100m Jumamosi usiku.
Hii ina maana kwamba bingwa huyo wa
dunia mara 19, ambaye Lord Coe alimfananisha na Muhammad Ali, aliondoka kwa
njia isiyo ya kawaida - akisaidiwa kuondoka uwanjani na wenzake, akiwa hawezi
kusimama vyema wima baada ya kuumia.
"Kwangu, sidhani mashindano haya
yatabadilisha yote niliyoyafanya,2 aliongeza.
"Nakumbuka baada ya kushindwa mbio
za 100m, kuna mtu alinijia na kuniambia, 'Usain, usiwe na wasiwasi, Muhammad
Ali alishindwa pigano lake la mwisho, hivyo usisikitike sana kuhusu hilo'.
"Nimedhihirisha ustadi wangu,
mwaka baada ya mwaka, katika kipindi changu chote nilichoshiriki mbio hizi.
Nilikuwa nasema kwaheri kwa kila kitu. Nilikuwa karibu kulia. Nilikaribia sana,
lakini machozi hayakutoka."
No comments:
Post a Comment