Waziri
Mkuu wa mstaafu, Frederick Sumaye ameingia matatani tena baada ya
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kumpokonya shamba lake lenye ukubwa wa
ekari 326 kwa madai ya kutoendelezwa huku ikisema Rais John Magufuli
ameridhia hatua hiyo.
Hili
ni shamba la pili Sumaye kunyang’anywa baada ya ekari 33 zilizopo eneo
la Mabwepande kuchukuliwa Novemba mwaka jana huku Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Ally Hapi akisema Serikali ilifikia uamuzi huo baada ya
kiongozi huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza kama notisi ya siku 90
ilivyoeleza.
“Oktoba
28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi
ya shamba namba 3,074 lililopo Mabwepande. Shamba hilo lilikuwa na hati
namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline
Sumaye,” alisema Hapi.
Jana,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero, Frolent Kyombo alisema Rais
Magufuli amekubali kufutwa kwa umiliki wa shamba hilo kupitia ilani ya
ubatilisho ya Mei mwaka huu.
Kabla
ya kupokonywa shamba hilo, Kyombo alisema Sumaye alipewa notisi ya siku
30 iliyomtaka kueleza sababu za kutoendeleza matumizi ya shamba hilo
kwa shughuli za kilimo kama lilivyosajiliwa lakini hakutoa sababu
zilizoweza kushawishi kutofanyika kwa mabadiliko hayo.
“Hatua
ya pili, tukatoa ilani ya ubatilisho wa shamba hilo, kuna maelezo
alitoa lakini tuliona hayakuwa na uzito, tukayatupilia mbali, shamba
hilo alikuwa anaendesha shughuli za kilimo pamoja na ufugaji. Alikuwa
anatumia asilimia 15 hadi 20 tu ya shamba lote,” alisema Kyombo.
Alisema
mbali na kutumia sehemu ndogo huku nyingine ikiwa haitumiki, Mwenyekiti
huyo wa Chadema Kanda ya Pwani alikuwa amekiuka Sheria ya Mipango Miji,
namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999.
“(Sumaye)
alitakiwa kutumia shamba hilo kwa ajili ya kilimo tu na siyo kwa
shughuli nyingine za ufugaji, hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria hizo.
Kwa hiyo mchakato umeashaanza wa kuligawa shamba hilo kwa wananchi na
tunategemea miezi minne ijayo tutakuwa tumemaliza taratibu zote,” alisema.
Desemba
15, 2015, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi alitangaza kiama kwa watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza
huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki.
Akizungumza
kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, alisema kuna
watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi
na mbaya zaidi, wanayatumia kukopa fedha benki.
No comments:
Post a Comment