WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya
wakimbizi ya Ulyankulu waache kujihusisha na matukio ya uhalifu.
Ametoa
onyo hilo jana mchana (Ijumaa, Agosti 11, 2017) wakati akiwahutubia
mamia ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya VETA, wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Amesema
matukio ya ujambazi, mauaji na umiliki wa silaha yanayofanyika kwenye
tarafa hiyo ni mengi ikilinganishwa hali ilivyo kwenye maeneo mengine ya
mkoa huo.
"Taarifa
nilizonazo zinaonyesha katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na
matukio ya mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki wa silaha nao
unatisha. Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four
mbili."
"Tulikamata
pia risasi 714 za SMG zikiwa kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka
mafuta ya mawese. Pia risasi mbili za Mark Four zilikamatwa," amesema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amewataka wakazi hao ambao baadhi yao wamepewa uraia na wengine
bado ni wakimbizi waonyane wanapokutana kwenye vikao vyao kwa sababu
matendo yao yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi. "Ni vema
mkikutana kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana," amesema Waziri
Mkuu.
"Ninawasihi
matukio haya myadhibiti la sivyo mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo
wenu. Bunduki na risasi zinakuja kufanya nini wakati nyie mko maeneo
salama? Mauaji ya nini? Kama kuna tatizo limekupata, muone mwenyekiti
wa kijiji, atakusaidia," alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi yao ambao wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila kufuata utaratibu.
"Hatuzuii
mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni lazima mfuate taratibu.
Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini pia tudumishe urafiki wa
nchi zetu mbili za Burundi na Tanzania," aliongeza.
Mapema,
Mbunge wa jimbo la Ulyankulu, Bw. John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu
afuatilie suala la upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba
wasaidiwe ili kata tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe
kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment