Wednesday, August 16, 2017

JAPANI YAKUBALI KUMALIZA FOLENI DAR. .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 15 Agosti, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Mbunge na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Ichiro Aisawa Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Katika Mazungumzo hayo Mhe. Ichiro Aisawa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri, kupambana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo, juhudi ambazo zinasaidia kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.
Mhe. Ichiro Aisawa ambaye ametembelea baadhi ya miradi inayojengwa hapa nchini na kampuni za Japan ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za juu (Flyover) wa TAZARA na Mradi wa kuzalishaji umeme kwa gesi wa Kinyerezi amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa kampuni hizo zitafanya kazi nzuri na zitakamilisha kazi kama ilivyopangwa.
Pia Mhe. Ichiro Aisawa amesema baada ya kuona changamoto ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam amebaini kuwa nchi yake bado inahitaji kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam na ameahidi kufikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Shinzo Abe.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Ichiro Aisawa kwa kuja Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo, na itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi Jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na zaidi ya njia nane, ujenzi wa barabara ya TAZARA, ujenzi wa Daraja la Gerezani njia nne, na barabara ya Bendera tatu hadi Kamata.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Ichiro Aisawa ambaye ni mwakilishi wa wabunge wa Japan wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Japan kuja kuwekeza hapa nchini na ameahidi kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wao unalindwa kama itakavyofanya kwa kampuni ya kutengeneza rangi ya Kansai Plascon ambayo awali ilijulikana kama Sadolin, na kampuni inayozalisha Betri za Panasonic hapa nchini, ili uwekezaji huo ulete manufaa hapa nchini.
“Naomba unifikishie ujumbe kwa Waziri Mkuu Shinzo Abe kuwa Tanzania inamshukuru kwa ushirikiano huu mkubwa, tunamkaribisha sana Tanzania na kwa kuwa Serikali yetu imehamia Dodoma tutafurahi sana kama Japan itaweka alamu ya urafiki wetu kwa kutujengea barabara za Dodoma mjini, iwe ni flyover au kilometa 20 za barabara, sawa tu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida.

No comments:

Post a Comment