Monday, August 21, 2017

Rais Buhari asisitiza umoja hotuba ya kwanza baada ya kurejea Nigeria

Buhari

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameihutubia taifa baada ya kuwa Uingereza kwa miezi mitatu akipata matibabu.

Katika hotuba yake kwenye televisheni, Buhari, mwenye umri wa miaka 74, alisema "alifadhaishwa" na wito wa kuigawanya Nigeria, akiwahimiza Wanigeria kuwa na umoja.
Lakini rais hakufichua anaugua wapi. Hii ilikuwa mara yake ya pili kuchukua likizo kwa sababu za kimatibabu mwaka huu.
Raia wengi wa Nigeria walimwomba ajiuzulu wakati hakuwepo nchini, wakisema hakuwa na uwezo wa kuiongoza nchi.
Wengine wamemuuliza kusema anaugua nini huku uvumi ukiongezeka kuhusu uwezekano wake kuwania urais tena mwaka 2019.

Makamu wa Rais Yemi Osinbajo amekuwa akiwajibika wakati Buhari amekuwa Uingereza, lakini Buhari sasa amerejelea kazi yake kama rais.
Akizungumza siku mbili baada ya kurudi kwake, Buhari alisema kuwa maoni kuhusu kuwaganywa kwa Nigeria "yamevuka mstari wa rangi nyekundu".
"Umoja wa Nigeria upo na sio wa kujadiliwa," alisema. "Hatuwezi kuruhusu watu wasiowajibika kuleta shida."
Rais pia alizungumzia vita vya kikabila nchini, akisema vinasababishwa na "wahalifu wa kisiasa".
Kuna watu ambao wamekuwa wakiitisha kuanzishwa kwa nchi tofauti maeneo ya kusini-mashariki inayojulikana kama Biafra huku vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu, Boko Haram vikiendelea katika maeneo ya kaskazini.

Raia wa Nigeria walikuwa wanatumai kupata habari kuhusu kile kinachomfanya rais wao kuugua lakini ofisi ya rais imekataa kufichua lolote.
Licha ya kuwa imesisitizwa kuwa Buhari yuko sawa na mwenye afya, alionekana mnyonge akiwasalimia wanasiasa jumamosi.
Ana nafuu kidogo - mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa mwezi Mei kabla hajaelekea Uingereza, alipowapokea wasichana 82 wa Chibok waliokuwa wameachiliwa. Hakuweza kusimama.
Jumatatu alijikakamua kuonyesha kuwa yuko tayari kuiongoza nchi. Lakini wengi bado wanauliza maswali kuhusu uwezo wake wa kuiongoza nchi.
Wakati Buhari alikwenda London mara ya kwanza - Juni 2016 - ofisi yake ilisema ni kwa sababu anaugua sikio.
Taarifa rasmi iliyotolewa mwezi Machi 2017 ilisema kuwa rais amekuwa "kwenye likizo, na alichukua nafasi hiyo kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu".
Wapinzani wake wakuu katika uchaguzi wa Nigeria wa 2015 walidai alikuwa na saratani ya tezi dume, lakini alikanusha.

No comments:

Post a Comment