Usain Bolt aliumia
na kushindwa kumaliza mbio zake za mwisho za ubingwa wa dunia jijini
London, na mwanariadha mwenzake Yohan Blake anasema huenda kucheleweshwa
kwa mbio hizo kulimwathiri.
Bolt alipata mkakamao wa misuli na
kulazimika kuondoka uwanjani alipokuwa akikimbia mbio za kupokezana
vijiti za 4x100m ambazo timu ya Uingereza ilishinda.
Yohan Blake alisema hilo: "Mbio zilicheleweshwa dakika 10, tuliwekwa tukisubiri kwa dakika 40. Ilitushangaza sana.
"Watuweka muda mrefu sana tukisubiri."
Bolt
alikuwa ametumai kwamba angemaliza maisha yake ya ukimbiaji kwa
kushinda dhahabu mbili mashindano hayo ya London lakini ameondoka sasa
na nishani ya shaba pekee aliyoishinda kwenye mbio za mita 100 wikendi
iliyopita.
Sekunde chache baada yake kupokezwa kijiti awamu ya mwisho ya mbio hizo, alitatizima na kuanguka sakafuni.
Daktari wa timu ya Jamaica Kevin Jones amethibitisha kwamba Bolt alipatwa na mkakamao wa misuli ya mguu wake wa kushoto.
"Ilikuwa
dakika 40 na walitoa nishani kwa washindi wa mbio mbili kabla yetu
kukimbia," aliongeza bingwa wa zamani wa mbio za mita 100 Blake.
"Tulikaa tukipasha misuli joto na kusubiri, kisha tunapasha misuli moto tena na kusubiri. Nadhani hilo lilitwathiri.
"Inauma kumuona jagina halisi, bingwa halisi akiingia uwanjani na kutatizika kwa namna hiyo."
Bingwa
wa mbio za 110m za kuruka viunzi Omar McLeod, aliyeongoza timu ya
Jamaica ambayo ilikuwa imeshinda ubingwa wa mbio za 4x100m katika makala
manne yaliyopita ya ubingwa wa dunia, alikubaliana na mtazamo wa Blake.
Sherehe za kumuaga Mo Farah baada yake kumaliza
nafasi ya pili mbio za 5000m zilionekana kuchelewesha ratiba, na pia
Farah alikabidhiwa nishani yake kabla ya fainali ya mbio hizo za
kupokezana vijiti.
"Inauma sana. Nilijitolea kabisa na nilitaka
sana kumuona Usain akiondoka kwa ushindi, au hata kama ingekuwa nishani
tu. Inashangaza bwana, tulisubiri muda mrefu. Nilikunywa chupa mbili za
maji.
"Lakini jina la Usain Bolt litasalia kukumbukwa."
Mshindi
wa mbio za 100m Justin Gatlin alisema Bolt 'ndiye bado bora zaidi
duniani' baada yake kushinda nishani ya fedha na timu yake ya Marekani.
Alikiri kwamba huenda hali ya hewa ilimwathiri Bolt.
"Nafikiri
ni hali ya hewa iliyomsababishia Bolt jeraha. Lakini bado ndiye bora
zaidi duniani. Huu ni wakati wa kuaga, naanza kumkosa tayari. Sehemu ya
kupashia misuli moto, huwa tunaheshimiana na tulisalimiana. Usain Bolt
ni mwanariadha mzuri sana."
Nishani alizoshinda Usain Bolt | |
---|---|
2007 Ubingwa wa Dunia | Fedha (200m), Fedha (4x100m kupokezana vijiti) |
2008 Olimpiki | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m) |
2009 Ubingwa wa Dunia | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m kupokezana vijiti) |
2011 Ubingwa wa Dunia | Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m relay) |
2012 Olimpiki | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m kupokezana vijiti) |
2013 Ubingwa wa Dunia | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m kupokezana vijiti) |
2015 Ubingwa wa Dunia | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m kupokezana vijiti) |
2016 Olimpiki | Dhahabu (100m), Dhahabu (200m), Dhahabu (4x100m kupokezana vijiti) |
2017 Ubingwa wa Dunia | Shaba (100m) |
No comments:
Post a Comment