Mkurugenzi wa mawasiliano katika ikulu ya White House Anthony Scaramucci amefutwa kazi chini ya siku 10 baada yake kuteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo.Scaramucci, ambaye amehudumu kwa kipindi kirefu katika Wall Street, alikuwa amekosolewa sana baada yake kumpigia simu mwanahabari mmoja kuwasema wahudumu wenzake katika ikulu.
Mkuu wa utumishi wa umma wa Bw Trump Reince Priebus na msemaji wake Sean Spicer wote walijiuzulu kutokana na uteuzi wa Scaramucci.
Uamuzi wa kumfuta kazi umefanywa na mkuu mpya wa utumishi wa umma wa Trump, John Kelly, ambaye aliapishwa mapema leo Jumatatu.
Taarifa fupi ya sentensi tatu kutoka White House imesema: "Anthony Scaramucci atauacha wadhifa wake kama Mkurugenzi wa Mawasiliano wa White House.
"Bw Scaramucci aliona ni vyema kumpa Mkuu wa utumishi wa umma John Kelly mwanzo mpya na uwezo wa kuunda timu yake. Tunamtakia kila la heri."
Awali, Bw Trump alikuwa ameandika kwenye Twitter kuhusu takwimu za nafasi za kazi na ujira, na akasisitiza kwamba hakukuwa na mzozo wowote White House.
Bw Scaramucci alikuwa awali amejiringa kwamba huwa anaripoti moja kwa moja kwa rais badala yake kupitia kwa mkuu wa utumishi wa umma.
Reince Priebus alijiuzulu Ijumaa baada ya Bw Scaramucci kuandika ujumbe kwenye Twitter na kisha kuufuta, ambapo wengi waliufasiri kama tuhuma na tishio dhidi ya Priebus.
Alimpigia pia simu mwanahabari na kumtusi Priebus akisema ni mtu mwenye wasiwasi mwingi na pia akamtuhusu kwa kuvujisha siri kwa wanahabari.
Alisema pia mambo mabaya kwenye mawasiliano hayo ya simu kuhusu mwanamikakati mkuu wa Trump, Steve Bannon.
CHANZO :BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment