Thursday, July 20, 2017

AGIZO LA WAZIRI KAIRUKI KWA OFISI ZA SERIKALI KUHUSU UHAMISHO WA WAFANYAKAZI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki  amezitaka Taasisi za Serikali kuratibu suala la uhamisho wa watumishi wa umma kwa makini pale inapohitajika kufanya hivyo Ili kuepuka kero na usumbufu kwa watumishi.
Waziri Kairuki amesema hayo jana katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala eneo la Segerea, jijini Dar es Salaam.
 
Mhe. Kairuki alisema uhamisho lazima ufanyike kwa mtumishi wa umma endapo kukiwa na sababu za msingi sana. “Naomba ieleweke kuwa uhamisho una taratibu zake hivyo kila mwajiri ni mwajiri akazifuata.” Mhe. Kairuki alisisitiza.
Aliongeza kuwa imebainika wapo baadhi ya watumishi wa umma wanawasilisha sababu mbalimbali kwa waajiri kuomba kuhama wakiwa na nia ya kukwepa kukaguliwa sifa zao za elimu.
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa uhamisho usifanyike kwa mtumishi ambaye anaonekana kuwa na matatizo.
“Baadhi ya waajiri wamekuwa na tabia ya kuwahamisha watumishi wa umma ambao wameonekana kuwa na tatizo na kuwahamishia sehemu nyingine, uhamisho wa namna hii haukubaliki, tatizo la mtumishi linatakiwa kufanyiwa kazi kwenye kituo chake cha kazi na sio kupeleka tatizo sehemu nyingine.” Mhe. Kairuki aliongeza.
Mhe. Kairuki yupo katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama ambapo leo ni siku ya tisa akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala-Segerea kwa kukutana na watumishi wa umma wa kada zote katika vikao kazi.
Waziri Kairuki katika vikao kazi alihimiza watumishi wa umma nchini kubadili mtindo wa maisha, kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kujiepusha na ugonjwa wa UKIMWI, na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY).
Lengo la kukutana na watumishi wa umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment