Tuesday, July 25, 2017

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WAKUU WA MIKOA YA MBEYA NA SONGWE .





Katika kuhakikisha kuwa Serikali inamaliza migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wawekezaji, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza wakuu wa mikoa ya Mbeya na Songwe kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita, kati ya uongozi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya na wananchi wa kijiji cha Nanyala, Wilayani Mbozi.




Mgogoro huo, umetokana na Kiwanda cha Saruji Mbeya, kupewa eneo la kijiji hicho chenye ekari 2,315 na uongozi wa mkoa wa Mbeya bila ya makubaliano na wanakijiji hali iliyosababisha wagome kuondoka.



Majaliwa ametoa agizo hilo jana  mara baada ya wananchi wa kijiji hicho kuzuia msafara wake kwa lengo la kumuelezea changamoto yao ya kudhulumiwa ardhi yao na kukabidhiwa kwa muwekezaji bila ya kushirikishwa.



Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli ni sikivu na inawajali wanyonge ndio maana amesimama ili aweze kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi, hivyo amewaomba waendelee kuiamini na watarudishiwa ardhi yao.



Vile vile, Majaliwa  ameiagiza Kampuni ya Saruji Mbeya kuondoa kesi iliyoifungua mahakamani dhidi ya wananchi wa eneo hilo, ili waweze kukutana na Serikali pamoja na wananchi hao kwa ajili ya kujadili namna bora ya uwekezaji katika eneo hill.


“Hatuzuii kiwanda kufanya kazi ila tunataka mkubaliane na wananchi kwanza ili kuondoa migogoro, Wananchi wanahitaji viwanda ila si kwa migogoro, Wananchi nawaomba muendelee kuwa na amani na hakuna atakayechukua ardhi yenu bila ya ridhaa yenu.”alisema Majaliwa.



Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe alimshukuru Waziri Mkuu kwa kulitolea tamkoa suala hilo na kwamba atakutana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo ili wananchi waweze kuishi kwa amani katika ardhi yao.

No comments:

Post a Comment