Mbunge
wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tundu Lissu jana aligoma kutoka katika chumba cha
mahakama kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa kuna baadhi ya polisi wametumwa
kumkamata kiongozi huyo. .
Lissu
alifika mahakamani hapo jana asubuhi kwa ajili kusimamia kesi ya
migogoro ya ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iliyokuwa
ikisikilizwa na Hakimu Proches Mushi.
Katika
kesi hiyo, Kamati ya Utendaji ya CWT wilaya imefungua kesi dhidi ya
Katibu Mkuu wa CWT, Yahaya Msulwa wakimtuhumu kwa matumizi mabaya
madaraka.
Hata
hivyo wakijadili muda wa kurudi tena kwa kesi hiyo, Lissu ambaye pia ni
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) alisema kuna polisi
waliovalia kiraia waliokuwa wakimngojea nje ili wamkamate na
kumsafirisha kwenda Dar es Salaam.
Habari
za kutaka kukamatwa kwa Lissu zilisikika asubuhi katika mitandao ya
kijamii baada ya kutumiwa ujumbe kuwa kuna maaskari waliovalia kiraia
wanataka kumkamata.
“Mheshimiwa
naomba kesi hii isisomwe tarehe 23 kwa sababu sitakuwepo nchini,
natarajia kwenda Uganda kwenye kikao cha vyama vya Afrika Mashariki vya
mawakili,”alisema na kuongeza:
“Lakini
pia nimepewa taarifa kuwa hapo nje kuna polisi wananisubiri nikitoka
wanikamate na kunisafirisha kwenda Dar es Salaam hivyo huenda tarehe
hiyo (Julai 23) nisiwe huru kuhudhuria kesi.”
Akijibu maombi hayo Mushi alisogeza kesi hiyo hadi Septemba 27-29 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Mara
baada ya kesi kuahirishwa, Lissu akafanya mkutano na waandishi wa
habari ndani ya ukumbi wa mahakama hiyo na kudai hatatoka mahakamani
hapo ili aone kama polisi wana uwezo wa kuingia na kumkamata.
“Leo
asubuhi nimepata taarifa kutoka Dar es Salaam kwa mama watoto wangu
kwamba polisi walikuja nyumbani kwangu kunitafuta na wakaelezwa kwamba
yuko Dodoma kwa muda wa siku tatu,” alisema.
“Baada
ya hapo wasamaria wema walinitaarifu kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam
limewaomba wenzao wa Dodoma wanikamate pindi tu nitakapotoka hapa na
kunirejesha Dar es Salaam.”
Alipoulizwa
sababu inayofanya polisi watake kumkamata, Lissu amesema ni kutokana na
maoni yake aliyoongea juzi ya kuukosoa uongozi wa Rais Magufuli.
“Rais
Magufuli na chama chake wameshindwa siasa na wanachofanya sasa ni
kutumia mabavu lakini wao kama Chadema kamwe hawataogopa wala kukaa
kimya kwani kazi yao si kumsifia Rais bali ni kumkosoa anapofanya
vibaya,”amesema.
Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema hakuna sheria yoyote
inayowaruhusu polisi kumkamata wakili akiwa katika shughuli zake
mahakamani.
“Nakaa
nione kama watavunja sheria ya kuja kunikamatia hapa hapa mahakamani.
Nimeshazoea kukamatwa tangu mwaka huu uanze nimekamatwa mara nne,”alisema.
Baada
ya kukaa mahakamani kwa saa nne, alifika Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma, Lazaro Mambosasa na kumweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi
Dodoma halina taarifa yoyote wala mpango wowote wa kumkamata.
“Hatujapokea
taarifa yoyote wala maelekezo yoyote ya kukukamata kutoka makao makuu.
Hata ingekuwa hivyo tungeshakukamata kwa sababu muda wa mahakama
umekwisha. Kwa sasa hivi yamebakia majengo tu kwa hiyo uwe huru uendelee
na shughuli zako,” Mambosasa alimwambia mbunge huyo.
Baada ya Mambosasa kuondoka katika mahakama hiyo, Lissu naye aliondoka katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment