Saturday, July 29, 2017

KATIKA SIASA MAALIM ATETA TENA JUU YA TANZANIA NI KWELI ASEMAYO


Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kujaza nafasi nane za ubunge wa viti maalumu za CUF, kambi ya katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad imesema bado inawatambua wabunge waliovuliwa uanachama na kambi pinzani na kutaka jumuiya ya kimataifa iiwekee vikwazo Tanzania.

Kambi inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba, ambayo inatambuliwa na vyombo vya Serikali, ilitangaza kuwavua uanachama wabunge wanane wa viti maalumu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Waliopoteza ubunge ni Halima Ali Mohamed, Khadija Salum Ally, Salma Mohamed Mwassa, Miza Bakari Haji, Rais Abdallah Mussa, Riziki Shahari Mngwali, Saumu Heri Sakala na Severina Mwijage.

Siku moja baada ya kambi ya Lipumba kupeleka majina hayo, Spika wa Bunge alikubaliana na uamuzi huo na kutangaza nafasi hizo kuwa wazi na siku iliyofuata Tume ya Uchaguzi ikatangaza wabunge wapya, uamuzi “wa mwendokasi” ambao umeishangaza kambi ya Maalim Seif ambayo imeupinga.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha dharura cha Baraza Kuu kilichofanyika ofisi ndogo za CUF zilizopo Vuga mjini Zanzibar, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za CUF wanachama hao bado ni wabunge.

Alisema kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 45 kati ya 52.

Katibu mkuu huyo alisema wabunge hao wataendelea na wadhifa huo kwa kuwa waliteuliwa na vikao halali vya Baraza Kuu lililo upande wake, ambalo ndilo halali kwa mujibu wa katiba na sheria za CUF.

Pia, alisema baraza hilo lina wajumbe 52, na kati yao 25 wanatoka Tanzania Bara na 27 wanatoka Zanzibar na litakuwa hai hadi mwaka 2019. 

“Baraza Kuu la uongozi halijakutana mahali popote Jumapili Julai 23 na kufanya uamuzi wowote wa kuwafukuza uanachama wabunge wanane na madiwani wawili wa CUF kama inavyodaiwa na mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba na kikundi chake,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema kufukuzwa kwa wabunge na madiwani hao si mpango wa Lipumba pekee, bali ni mpango kabambe uliosukwa na dola kwa kushirikiana naye.

Alisema ushahidi wa hilo ni kufukuzwa kwao na Lipumba ambaye ni mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na papo hapo Spika wa Bunge kuridhia na NEC kutangaza majina ya wateule wa kujaza nafasi hizo.

“Baraza Kuu limeshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kujifedhehesha na kujiaibisha kwa kusema uongo kwa Watanzania kwamba eti alijiridhisha kwamba wabunge hao wanane wamefukuzwa uanachama na chama chao na kudai kuwa tayari wamekosa sifa za kuendelea kuwa wabunge,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema kutokana na hali hiyo ni vyema Spika akajiuzulu kutokana na kwenda kinyume cha utaratibu wa uendeshaji wa Bunge.

Alisema baraza hilo limemtaka kuandika barua kwa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), katibu wa umoja wa mabunge ya jumuiya ya Madola (CPA), katibu wa umoja wa mabunge ya duniani (IPU) kuhusu suala hilo.

Kuhusu NEC, alisema ni dhahiri imezidi kupoteza sifa na kujionyesha wazi kuwa haipo huru.

“Hata kama hawa wabunge wangekuwa wamefukuzwa kweli na baraza linalotambulika, lazima tume ifuate utaratibu uliopo kwa kuchukua orodha ya majina ya watu iliyowasilishwa ofisini kwake mwaka 2015 kujaza nafasi za uteuzi, orodha yetu ipo halali mbona hawa walioteuliwa hawamo ndani ya orodha yetu,” alihoji Maalim Seif.

Waliopitishwa na NEC ni Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainabu Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredia Apolinary Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.

Alisema kutokana na kuvunjwa katiba na sheria za nchi zilizopo ni vyema sasa jumuiya ya kimataifa ikasitisha misaada kwa Serikali ya Tanzania hadi hapo itakapokuwa tayari kufuata Katiba na hasa katika masuala ya siasa.

Alisema vitendo vinavyofanyika ni dhahiri vinaonyesha kuwepo dhuluma na udhalilishaji wa demokrasia kwa vyama vya upinzani.

“Baraza la uongozi linaunga mkono wito uliotolewa na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu kwa jumuiya ya kimataifa kuibana Tanzania kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na kuitenga kisiasa na kidiplomasia hadi hapo watawala watakapoamua kuheshimu katiba, sheria, misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu na utawala bora,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema anajiamini na yupo tayari kukamatwa kama utawala ukiona aliyosema hayafurahishi.

Alisema kukaa jela itakuwa si mara ya kwanza, akidai kuwa ameshawahi kukaa na wala haikuwa kitu, hivyo akipelekwa tena itakuwa ni kama jambo la kawaida tu kwa upande wake.

No comments:

Post a Comment