Februari 2014, Ngeleja
ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema (CCM) aligaiwa Sh. milioni 40.4 na
mfanyabiashara maarufu James Rugemalira ambaye mwanzoni mwa mwezi alifikishwa
mahakamani akikabiliwa na
mashtaka 12, yakiwamo ya kughushi na utakatishaji fedha.
mashtaka 12, yakiwamo ya kughushi na utakatishaji fedha.
Waziri wa Nishati na Madini
wa zamani Ngeleja ni mmoja kati ya watu waliopokea mgawo wa fedha zinazodaiwa
kuwa zao la kashfa ya Tegeta Escrow, lakini akatangaza kuzirejesha kwa TRA
Jumatatu iliyopita.
Hata hivyo, wakati Ngeleja
akithibitisha kwa risiti mbele ya waandishi wa habari kuziingiza fedha hizo
katika akaunti ya TRA, mamlaka hiyo imesema haizitambui. TRA imesema haina
mpango wowote wa kufuatilia fedha hizo kwa sababu shughuli yake ni kukusanya
kodi.
Akizungumza na Nipashe
mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TRA, Richard Kayombo alisema
mamlaka hiyo inahusika na kuhakikisha serikali inakusanya kodi stahiki na siyo
urejeshaji wa fedha za kashfa kama Escrow.
Kayombo alitoa ufafanuzi huo
wakati alipoulizwa na Nipashe juu ya utaratibu rasmi uliopo wa urejeshaji wa
fedha hizo endapo wanufaika zaidi wa mgawo wa Rugemalira watataka kufuata nyayo
za Ngeleja.
Akifafanua zaidi juu ya
suala hilo, Kayombo alisema TRA haihusiki na fedha zilizochotwa kwenye akaunti
ya Tegeta Escrow kwa kuwa hazikuwa mali yake.
Aidha, Kayombo alisema TRA
haiwezi kuzizungumzia fedha hizo kwa kuwa hazijawahi kuwa mali yake na
kuelekeza watafutwe wenye fedha hizo kwa ufafanuzi zaidi.
“Fedha za Escrow zinaihusu
vipi TRA? Tunawezaje kukaa na kuzungumzia fedha ambazo si zetu?” Alisema
Kayombo. “Mimi nashauri watafutwe wenyewe wazungumze kama wanataka kurejesha…
siyo sisi.”
Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tundu Lissu aliiambia Nipashe wiki iliyopita kuwa uamuzi wa
Ngeleja kupeleka fedha za hizo TRA unazua maswali zaidi kwa kuwa alipewa na
Rugemarila, na viongozi wa awamu ya nne ya serikali walisema siyo za umma bali
mtu binafsi.
Lakini akizungumza jijini
Jumatatu iliyopita Ngeleja alisema amerejesha mgawo huo kwa TRA kwa kuwa pamoja
na sababu nyingine, ili kujiweka kando na kashfa.
Alisema aliyetoa mgawo huo
ameshakamatwa na Takukuru na ana kesi inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu.
Huku akionyesha stakabadhi
ya malipo ya Benki ya CRDB tawi la Tower, Ngeleja alisema pia “nimeamua
kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa, kwa vile
hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa au
tuhuma hizo.”
“Nimesononeshwa na
kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma.”
Alisema alipokea mgawo huo Februari
12, 2014 na Januari 15, 2015 alilipa kodi kwa TRA kiasi cha Sh. 13,138,125
ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya msaada huo aliopewa.
Hakusema ni kwa nini ulipita
muda mrefu kati ya kupokea na malipo ya kodi.
Baada ya Ngeleja kurejesha
fedha hizo palikuwa na wito kutoka kwa wanasiasa na wanaharakati waliotaka wote
waliopata mgawo huo kurejesha fedha hizo kwa TRA kama alivyofanya waziri huyo
wa zamani.
MASHTAKA 12
Rugemalira na mwenzake,
mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power (PAP), Harbinder Singh Sethi walisomewa
mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 3.
Mashtaka hayo ni pamoja na
ya kugushi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya dola zaMarekani milioni
22.1 na Sh. bilioni 309.4 kwa serikali.
Novemba 26, 2014, Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwasilisha mjini Dodoma ripoti ya uchunguzi
wa kashfa Tegeta Escrow ambapo ilisema Sh. bilioni 306 zilichotwa kutoka Benki
Kuu kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa kamati hiyo
wakati huo, Zitto Kabwe alisoma ripoti na kulithibitishia Bunge kwamba viongozi
na wafanyakazi wa Serikali, wafanyabiashara, viongozi na taasisi za dini,
mabenki na watu binafsi walihusika katika ufisadi.
Ripoti ya PAC ilianika
orodha ya waliopata mgawo huo kuwa mbali na Ngeleja ni aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge ambao kila mmoja alipata Sh. bilioni 1.6.
Wengine ni ofisa katika
Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh. milioni 80, Jaji wa
Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa alipata Sh. milioni 404.25 na aliyekuwa mjumbe wa
Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Dk. Enos Bukuku, aliyepewa Sh.
milioni 161.7.
Katika ripoti hiyo Waziri wa
Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani
wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji
(TIC), Emmanuel Ole Naiko na Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Aloisius Mujulizi walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.
Wengine ni ofisa wa TRA,
Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usajili
wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko Sh. milioni 40.2, maaskofu Methodius
Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius Nzingirwa Sh. milioni 40.4, Padri Alphonce
Twimannye Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na
Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.
BAJETI WIZARA
Mgawo waliopata wabunge,
maofisa wa serikali na viongozi wa dini kutoka kwa Rugemalira unatosha bajeti
ya mwaka mzima ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Nipashe imegundua.
Katika miaka mitatu
iliyopita ya bajeti (2014/15, 2015/16 na 2016/17), wizara hiyo ambayo kwa sasa
iko chini ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe, ilitengewa bajeti ya Sh. bilioni
tatu kila mwaka, ikiongoza wizara zote 18 kwa kuwa na bajeti ndogo zaidi kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati wizara hiyo
ikiambulia Sh. bilioni moja (theluthi ya bajeti yake ya maendeleo) hadi
inapofika robo tatu ya mwaka wa bajeti katika miaka hiyo mitatu, imebainika Sh.
bilioni 4.77 zinazodaiwa zao la kashfa ya uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow walizopatiwa waheshimiwa hao zingetosha kugharamia kikamilifu
miradi ya maendeleo ya wizara hiyo kwa mwaka mzima na ‘chenji’
ya Sh. bilioni 1.7 ikabaki.
Katika mwaka uliopita wa
fedha, kwa mfano, kati ya Sh. bilioni tatu zilizotengwa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo, ni Sh. bilioni 1.19 tu
(asilimia 40) ndizo zilizokuwa zimetolewa hadi Aprili 30, mwaka huu kwa mujibu
wa Dk. Mwakyembe.
Chanzo: NIPASHE
No comments:
Post a Comment