Saturday, July 29, 2017

NEC YAZUNGUMZIA KUHUSU CUF.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefafanua juu ya uteuzi wa wabunge wapya wa Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Imesema kuwa imesikitishwa na kushangazwa na taarifa za Baraza Kuu la Taifa la chama hicho kwamba tume hiyo imekiuka kanuni zake katika uteuzi wa wabunge wanane wa chama hicho ili kujaza nafasi za wazi zilizotokea hivi karibuni.

Aidha, imesema chama husika kilipewa fursa ya kupendekeza na kilifanya hivyo, kabla ya NEC kuanika majina ya wabunge wapya wa CUF katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yamo katika taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani aliyoitoa jana jioni, akizungumzia tuhuma dhidi ya tume hiyo, inayodaiwa kukiuka kanuni katika uteuzi wa wabunge wanane wa viti maalumu wa CUF.

Sehemu ya Taarifa ya CUF katika mitandao ya kijamii inayoituhumu NEC inasema; “Kanuni walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi wa watu wa kujaza nafasi hizo zinasema uteuzi huo unafuata mpangilio wa majina, kama ulivyokuwa umewasilishwa na chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti maalumu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

“CUF ilipeleka orodha yake ambayo haihusishi majina yaliyotangazwa, hivyo ndiyo kusema hata kama hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama wabunge hao kingekuwa halali (jambo ambalo si halali kama ilivyokwishaelezwa hapo juu), basi kwa Kanuni za Tume yenyewe, watu wa kujaza nafasi hizo wasingekuwa hao waliotangazwa.”

Kailima, katika taarifa yake, alisema taarifa zinazotolewa katika mitandao zikihusisha NEC kukihujumu chama hicho ni za kushangaza na kwamba Baraza Kuu la Uongozi la CUF, linataka kuupotosha umma kuhusu utekelezaji wa kazi za Tume.

“Chama husika ndicho kinaweza kujua ni nani siyo mwanachama wa chama hicho kwa kipindi cha kujaza nafasi wazi inapotokea,” alieleza Kailima na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa majina manane yaliyopendekezwa na CUF kujaza nafasi wazi za wabunge wa viti maalumu ni miongoni mwa majina 55 yaliyowasilishwa na chama hicho kwa barua yenye kumbukumbu Namba CUF/AK/DSM/ KM/003/1A/2015/14 ya Septemba 28, 2015 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.

No comments:

Post a Comment