Wednesday, July 12, 2017

WAZIRI MPANGO AFUNGA KITUO CHA GBP KILICHOPO ENEO LA UWANJA WA NDEGE, DAR.





Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuamuru kituo cha Mafuta cha GBP kifungwe hadi hapo kitakapo funga mashine maalumu za kutolea risiti baada ya kubainika hakitumii ipasanyo mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi (EFD)

Dkt. Mpango amechukua hatua hiyo baada ya kujionea kituo hicho kikiwa na pampu nne za mafuta lakini kuna mashine moja pekee ya mkononi ya kutolea risiti jambo linasababisha wateja wao wengi kutopewa risiti na hivyo kuikosesha Serikali mapato yake na ni kinyume cha sheria za nchi.

“Sasa nawachukulia hatua ili liwe fundisho kwa wengine wote wanaouza mafuta nchini bila kufuata taratibu, na nitaanza na wewe, biashara yako isimame mpaka mashine zifungwe kwenye kituo chote na utekeleze mara moja,” alisema Dkt. Mpango

Katika ukaguzi wa Kituo cha Mafuta cha Puma, Dkt. Mpango amesifu utaratibu mzuri uliowekwa na kituo hicho kwa kufunga mashine maalumu za kutolea risiti zilizounganishwa na kila pampu za mafuta kitu ambacho ndicho Serikali inavitaka vituo vyote vya mafuta vitumie mfumo huo

“Kituo hiki kimezingatia sheria sheria kwa kufunga mashine kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali na hapa tunauhakika wa kupata fedha za kuwatumikia wananchi, kinyume kabisa na kituo cha mafuta nilichokifungia, hapa ndio ningeomba Watanzania wanunue mafutaĆ¢€ aliongeza Dkt. Mpango.

Ameiagiza Mamlaka ya mapato Tanzania-TRA kufanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokiuka maagizo ya Serikali yaliyowataka wafunge mashine hizo maalumu tangu mwaka uliopita.

Waziri wa Fedha na Mipango amewageukia wenye vyombo vya moto wanaonunua mafuta kwenye vituo vya mafuta kote nchini kudai risiti wanapopata huduma ya kuwekewa mafuta kwenye vituo hivyo ili kuokoa fedha za Serikali zinazoishia mikononi mwa wajanja wachache wanaokwepa kodi kwa makusudi na kuikosesha Serikali mapato yake.

Baadhi ya wananchi wamepongeza uamuzi wa Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango wa kufanya ziara za kushitukiza kwenye vituo vya mafuta na kutaka hatua hiyo iwe endelevu kwa maafisa wengine wa Serikali ili kukomesha vitendo vya wenye vituo vya mafuta kukwepa kodi ya Serikali.

Katika siku yake ya kwanza ya ziara za namna hiyo, Julai 10 mwaka huu, Dkt. Mpango alikifungia kituo cha Mafuta cha Mawenzi kilichoko Kigamboni, Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa kituo hicho kimefunga mashine maalumu za kutolea risiti za kielektroniki lakini hazitumiki na kuamuru kituo hicho kifungwe hadi kitakapo rekebisha kasoro hiyo na kuvionya vituo vya mafuta vya OilCom kufunga mashine za aina hiyo mara moja.

No comments:

Post a Comment