Wednesday, July 12, 2017

WEDNESDAY, JULY 12, 2017

  JAPAN YAKABIDHI KIWANDA CHA MAFUTA KWA CHAMA CHA USHIRIKA CHATO......KINAUWEZO WA KUZALISHA LITA 700 ZA MAFUTA KWA SIKU. 



Serikali ya Japan imekabidhi kiwanda cha kuchakata na Kuzalisha Mafuta ya Alizeti kwa chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko wilayani Chato Mkoani Geita chenye uwezo wa kuzalisha lita 700 za mafuta kwa siku.

Akikabidhi kiwanda hicho,Balozi wa Japani nchini Bw. Masaharu Yoshida amesema Serikali ya Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano huo baina ya nchi hizo mbili katika kuleta maendeleo kwa wananchi Tanzania.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk. Medard Kalemani aliyeshiriki kwenye makabidhiano hayo amesema serikali ya Japani licha ya kujenga kiwanda hicho Chenye Thamani ya Sh. 170 milioni, pia Japan inatekeleza ujenzi wa mradi wa soko la samaki la Kimataifa katika kijiji cha Kasenda litakalogharimu Sh. 320 milioni.

Awali mwenyekiti wa Chama cha Ushirika na Masoko, Elias Kaswahili na Meneja wa Mradi huo Faidaya Misango wamesema uzalishalishaji wa Mafuta ni mkubwa ukilinganisha na upatikanaji wa Alizeti na hivyo kutoa wito kwa wananchi kulima zao hilo ili kuwezesha kiwanda hicho kufanya kazi.

Aidha, kwa niaba ya Wananchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameipongeza serikali ya Japan ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Japan ni nchi ambayo imetajwa kuwa rafiki wa karibu na Tanzania na hii inajidhihirisha katika kutoa ufadhili wa miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya miundombinu ya barabara, masoko, reli na elimu.


LISSU ATAKA WOTE WALIOPATA FEDHA ZA ESCROW WAKAMATWE 

 



Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika TLS, Tundu Lissu amesema kuwa watu wote waliopata mgawo wa fedha hizo wakamatwe kwakuwa wameuthibitishia umma kuwa ni wala rushwa.

Lissu amesema kuwa kwa sasa hakuna ubishi kuwa watu hao ni wala rushwa na walitumia madaraka yao vibaya kujipatia fedha hizo na kuwa watu hao ni sehemu ya mafisadi ambao wamekuwa wakihujumu nchi.

Ameyasema hayo baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya awamu ya nne na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kurudisha Serikalini kiasi cha shilingi milioni 40.4 za mgawo wa Escrow hali ambayo imeibua mijadala mingi.

Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, juzi alisema kuwa amefikia hatua hiyo ya kuzikabidhi fedha hizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kujiweka kando na kashfa hiyo kwakuwa aliyempa ni mtuhumiwa.

“Sheria inasema kuwa ukikutwa umeiba unakamatwa unafikishwa kwenye vyombo vya dola ukikutwa na hatia unafungwa na fedha unarudisha, kwa hiyo hawa wote waliochukua mgawo huo wakamatwe wafikishwe katika vyombo vya dola na sio kurudisha tu hizo fedha hawa ni wezi,”amesema Lissu

Hata hivyo, ameongeza kuwa bila kujali nafasi ya watu hao katika jamii waliopata mgawo huo wanapaswa kwakuwa hata unapokuwa kiongozi wa dini hupaswi kula rushwa au kuchukua fedha za rushwa.

NGELEJA AELEZA KWANINI HAKUMRUDISHIA FEDHA ZA ESCROW RUGEMALIRA NA BADALA YAKE ALIZIPELEKA TRA 


Siku chache baada ya kutangaza kuwasilisha shilingi milioni 40 katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja amefafanua sababu za kutomrejeshea fedha huyo mfanyabiashara, James Rugemalira ambaye alimpa awali kama msaada.

Fedha hizo ni sehemu ya shilingi bilioni 306 zilizotolewa katika akaunti maalum ya Tegeta Escrow mwaka 2014 iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, fedha zizotolewa kimakosa wakati kesi ya mgogoro wa kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ikiwa bado haijatolewa maamuzi.

Kwa mujibu wa taratibu, fedha hizo zilipaswa kutolewa baada ya kesi husika kukamilika na pande zote mbili kukaa pamoja kukokotoa kiasi cha fedha ambacho kila upande ungepaswa kupata kwa mujibu wa maamuzi.

“Kwa mazingira halisi yanayomkabili aliyenipa msaada, mahali salama pa kurejesha hizo fedha sasa ni serikalini. Serikali itajua kuwa fedha hizo zinastahili kwenda kwa Rugemalira sasa au wasubiri hatima ya kesi,” Ngeleja anakaririwa na Gazeti la Mwananchi .

“Ningerudisha kwa Rugemarila watu wangeweza kuibua hoja kwamba labda napiga changa la macho tu,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo maarufu ambaye kampuni yake ya VIP Engineering ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya IPTL, pamoja na Mwenyekiti wa Pan African Power Solution (PAP), Harbinder Singh Seth wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na bado wako mahabusu.

Mgao wa fedha hizo pia uliwafikia Anna Tibaijuka aliyekuwa waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Andrew Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Methodiu Kilaini, Jaji John Ruhangisa na wengine.

MAJALIWA: HAKUNA KIJIJI TANZANIA KITAKACHOACHWA BILA YA UMEME

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai 11, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa.

Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa aliyasema hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga, Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Pia Waziri Mkuu amesema mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi.

Waziri Mkuu alisema huduma hiyo ni muhimu kwani mbali ya kutumiwa majumbani lakini pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati,shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.

Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Mhandisi, Johnson Mwigune alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangiwa katika vijiji hivyo atakuwa tayari ameanza kazi ya kusambaza umeme.

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, JULAI 12, 2017

No comments:

Post a Comment